MwananchiHabari ZaidiKitaifa ‘Wapenzi’ wauawa kwa kuchomwa na vitu vyenye ncha kali Dodoma
Dodoma. Katika tukio linalohusishwa na wivu wa mapenzi, watu wawili wanaosadikika kuwa ni wapenzi wameuawa kwa kuchomwa vitu vyenye ncha kali kifuani na tumboni na watu wasiofahamika ndani ya nyumba katika mtaa wa Msangalee jijini Dodoma.
Waliouawa ni dereva wa bodaboda, Dominick Kigula na mwanamke Esther Shiyang.
Alipoulizwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Martine Otieno amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanakusanya taarifa hizo ambazo watazitoa baadaye.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Ibenzi Ernest alithibitisha
kupokelewa kwa miili ya wawili hao ikiwa imechomwa chomwa na vitu vyenye ncha kali.
“Miili yao ilikutwa imechomwa na vitu vyenye nja kali. Bado wamehifadhiwa hapa (Chumba cha Kuhifadhia Maiti),” amesema.
Mwananchi lilipofika katika nyumba hiyo iliyopo karibu na reli ya kisasa (SGR) inapojengwa jana Julai 20, ilikuta damu zimetapakaa katika miongoni mwa vyumba na kwenye koridoo ya nyumba hiyo ilikuwa ya kupanga.
Tukio hilo lilitokea jana saa 11.00 asubuhi ambapo mlango wa chumba alichokuwa akiishi dereva bodaboda huyo ulivunjwa.
Kwa mujibu wa majirani, mwili wa mwanaume mmoja aliyefahamika kwa jina la Jongo ambaye ni dereva bodaboda aliyekuwa amepanga katika nyumba hiyo ulikutwa ndani ya chumba alichokuwa amepanga huku wa mwanamke ukiwa katika koridoo ya nyumba hiyo.
“Walikuwa wanasema walisikia tu sauti ya mpangaji mwenzao ikisema sasa ndugu yangu si tuelewane tu,” amesema mmoja wa majirani ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Akizungumza jana na Mwananchi, mmliki wa nyumba hiyo, Yusto Kandido alisema Jongo alikuwa mpangaji wake aliyehamia katika nyumba hiyo miezi mitano iliyopita.
“Sikushuhudia tukio hilo wala sikufahamu kama (marehemu) alikuwa na ugomvi na mtu wakati wote ambao ameishi katika nyumba yangu,” alisema.
Amesema yeye aliitwa na mmoja wa wapangaji wanaoishi kwenye nyumba hiyo na alipofika alikutana na tukio hilo la kusikitisha.
“Nivyofika hapa na kukutana na hilo tukio, nikabaki katika mshangao tu wala sikujua nini kilichofanyika katika nyumba yangu,“ amesema Kandido.
Taarifa zaidi zimeeleza kuwa, kabla ya mwanamke huyo kuanza uhusiano na dereva huyo wa bodaboda, alikuwa na bwana mwingine waliyeachana, lakini alikuwa akimfuatilia kila mara.