Mwigizaji wa filamu Bi Sonia afariki dunia
Dar es Salaam. Msanii wa filamu nchini Tanzania, Farida Sabu maarufu 'Bi Sonia' amefariki dunia.
Bi Sonia amewahi kuwika katika maigizo mbalimbali ya kundi la Kaole.
Taarifa ya kifo chake imethibitishwa leo Alhamisi Julai 21, 2022 na Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji, Chiki Mchoma.
Mchoma amesema mama Sonia amefikwa na umauti leo akiwa Zanzibar kwa mtoto wake aliyekuwa akimuuguza.
Mara ya mwisho msanii huyo alikuwa akionekana katika tamthilia ya 'Ndoano' iliyokuwa inaruka kituo cha Azam ambayo ilishirikisha wasaniii waliowahi kuigiza Kaole ikijulikana kama kundi la 'Return of Kaole.'
Kati ya wasanii hao ni pamoja na Blandina Chagula 'Johari', Kenny Muhsin Awadhi 'Dk Cheni', Kingwendu, Kisa, Ben Blanco na wengine wengi.
Msiba upo Zanzibar na atazikwa hukohuko.